SW

Waraka kwa Waroma

Waraka kwa Waroma ni kitabu kimojawapo cha Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo. Andiko hili ni barua ya Paulo wa Tarso kwa ushirika wa Wakristo katika mji mkuu wa Dola la Roma.

Mwanzo wa waraka huu katika Codex Alexandrinus.

Agano Jipya

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

. . . Waraka kwa Waroma . . .

Kati ya maandiko matakatifu ya Agano Jipya na ya Biblia kwa jumla, barua ya Mtume Paulo kwa Wakristo wa Roma ina umuhimu wa pekee uliokusudiwa naye mwenyewe.

Paulo alikaa Efeso karibu miaka mitatu, lakini moyo wake wa kimisionari haukutulia kwa sababu alikumbuka alivyotabiriwa atafanya kazi hata mbali zaidi. Ndiyo maana alitaka kwenda Ulaya magharibi, yaani Roma na halafu Hispania, nchi iliyohesabika kuwa mwisho wa dunia. Ila kabla ya kwenda huko alipanga kuwaletea Wakristo wa Yerusalemu mchango wa wenzao wa mataifa.

Basi, mwishoni mwa miezi mitatu aliyokaa Korintho (Mdo 20:2-3) akijiandaa kupanda meli, yaani mwanzoni mwa mwaka58, Paulo aliwaandikia Wakristo wa Roma ili kuandaa utume atakaoufanya katika jiji hilo.

Huko Ukristo uliingia toka mwanzo kabisa, ukiletwa na baadhi ya Wayahudi wengi walioishi Roma ambao walibatizwaYerusalemu kwenye Pentekoste ya mwaka 30 (Mdo 2:1-12).

Wayahudi wote walipofukuzwa na Kaisari Klaudio (49), Wakristo wa mataifa mengine wakabaki ndio wengi, nao wakaachana na masharti mbalimbali za dini ya Kiyahudi, kama yale kuhusu vyakula.

Muda mfupi baada ya Klaudio kufa (54), Wayahudi walianza kurudi, kumbe wale ambao kati yao walikuwa wamemuamini Yesu wakakuta mabadiliko hayo makubwa ndani ya Kanisa, nao wakajiona wamewekwa pembeni kidogo, kama si kudharauliwa na Wakristo wa mataifa.

Mtume Paulo akijua umuhimu wa Roma, mji mkuu wa ulimwengu wa zamani hizo, aliwaandikia Wakristo wa huko barua ndefu tena nzito kuliko zote. Alitaka kuwaeleza kwa maandishi ya mpango mafundisho yake kuhusu wokovu, kwa sababu walikuwa wamesikia habari tofautitofauti juu yake bila ya kukutana naye.

Pamoja na kuwaandaa hivyo wampokee vizuri, alichukua nafasi ya kuimarisha umoja wao ulioingia dosari.

Akiandika kwa utulivu mkubwa kuhusu mambo aliyokwishawaongelea kwa hasiraWagalatia, Paulo aliweza kuinua pande zote mbili za Kanisa hilo zielewe zaidi fumbo la mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wote, na hivyo ziheshimiane kwa upendo, ulio utimilifu wa Torati.

Hasa aliwaonya Wakristo wa mataifa wasidharau Wayahudi, kwa sababu hao bado ni wateule wa Mungu.

. . . Waraka kwa Waroma . . .

This article is issued from web site Wikipedia. The original article may be a bit shortened or modified. Some links may have been modified. The text is licensed under “Creative Commons – Attribution – Sharealike” [1] and some of the text can also be licensed under the terms of the “GNU Free Documentation License” [2]. Additional terms may apply for the media files. By using this site, you agree to our Legal pages . Web links: [1] [2]

. . . Waraka kwa Waroma . . .

Back To Top