SW

Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni

Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni mwa waadilifu wote wa duniani, toharani na mbinguni ndio chemchemi isiyoumbwa ya maisha ya Kiroho kadiri ya imani ya Wakatoliki, Waorthodoksi na wengineo.

Elizabeti wa Utatu ni kati ya watakatifu waliofurahia zaidi uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni mwao.

. . . Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni . . .

Kwanza Mungu yumo katika viumbe vyote kwa kuwa hana mipaka: “Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko” (Zab 139:7-8). “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi… hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu” (Mdo 17:24-28). Kwa hakika, Mungu anaona vyote, anadumisha vyote, na kuongoza kila kiumbe kitende jinsi inavyokifaa.

Lakini Maandiko yanasema pia juu ya uwemo wa pekee wa Mungu katika waadilifu. “Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yoh 14:23). Hayatakuja tu mambo yaliyoumbwa (kama vile neema inayotia utakatifu, maadili ya kumiminiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu), bali watakaokuja ni walewale wanaopenda, Baba na Mwana wasiotenganika na Roho Mtakatifu, ambaye Yesu alimuahidi na kumtuma wazi kwenye Pentekoste: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele… Ndiye Roho wa kweli… anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu…” (Yoh 14:15-17). Hao watakuja si kwa muda, bali watafanya makao yao ndani ya mwadilifu mpaka atakapodumu katika upendo.

Maneno hayo hayakuwahusu mitume tu: “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh 4:8). Huyo anaye Mungu moyoni mwake, lakini hasa Mungu anaye huyo ndani mwake akimdumishia si tu uhai wa kimaumbile, bali pia ule mpya wa neema na upendo. “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5). Hatukujaliwa tu upendo ulioumbwa, bali Roho Mtakatifu aliye Upendo-Nafsi. Hao wamo ndani mwetu, lakini tutafananishwa nao kikamilifu hapo tu tutakapopokea mwanga wa utukufu. “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? …Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe” (1Kor 3:16; 6:19). Hivyo Maandiko yanafundisha wazi kuwa Nafsitatu za Mungu zinaishi katika waadilifu wote.

. . . Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni . . .

This article is issued from web site Wikipedia. The original article may be a bit shortened or modified. Some links may have been modified. The text is licensed under “Creative Commons – Attribution – Sharealike” [1] and some of the text can also be licensed under the terms of the “GNU Free Documentation License” [2]. Additional terms may apply for the media files. By using this site, you agree to our Legal pages . Web links: [1] [2]

. . . Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni . . .

Back To Top